| Chapter 20 |
1 |
"Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu mwenye shamba la mizabibu, ambaye alitoka asubuhi na mapema kuwaajiri wafanyakazi katika shamba lake. |
2 |
Akapatana nao kuwalipa dinari moja kwa siku, kisha akawapeleka katika shamba lake la mizabibu. |
3 |
Akatoka mnamo saa tatu asubuhi, akaona watu wengine wamesimama sokoni, hawana kazi. |
4 |
Akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu, nami nitawapeni haki yenu.` |
5 |
Basi, wakaenda. Huyo mwenye shamba akatoka tena mnamo saa sita na saa tisa, akafanya vivyo hivyo. |
6 |
Hata mnamo saa kumi na moja jioni, akatoka tena; akakuta watu wengine wamesimama pale sokoni. Basi, akawauliza, `Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?` |
7 |
Wakamjibu: `Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri.` Yeye akawaambia, `Nendeni nanyi mkafanye kazi katika shamba la mizabibu.` |
8 |
"Kulipokuchwa, huyo mwenye shamba alimwambia mtunza hazina wake, `Waite wafanyakazi ukawalipe mshahara wao, ukianzia na wale walioajiriwa mwisho, na kumalizia na wale wa kwanza.` |
9 |
Basi, wakaja wale walioajiriwa mnamo saa kumi na moja, wakapokea kila mmoja dinari moja. |
10 |
Wale wa kwanza walipofika, walikuwa wanadhani watapewa zaidi; lakini hata wao wakapewa kila mmoja dinari moja. |
11 |
Wakazipokea fedha zao, wakaanza kumnung`unikia yule bwana. |
12 |
Wakasema, `Watu hawa walioajiriwa mwisho walifanya kazi kwa muda wa saa moja tu, mbona umetutendea sawa na wao hali sisi tumevumilia kazi ngumu kutwa na jua kali?` |
13 |
"Hapo yule bwana akamjibu mmoja wao, `Rafiki, sikukupunja kitu! Je, hukupatana nami mshahara wa denari moja? |
14 |
Chukua haki yako, uende zako. Napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. |
15 |
Je, sina haki ya kufanya na mali yangu nipendavyo? Je, unaona kijicho kwa kuwa mimi ni mwema?"` |
16 |
Yesu akamaliza kwa kusema, "Hivyo, walio wa mwisho watakuwa wa kwanza na wa kwanza watakuwa wa mwisho." |
17 |
Yesu alipokuwa anakwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani, na njiani akawaambia, |
18 |
"Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu, na huko Mwana wa Mtu atakabidhiwa kwa makuhani wakuu na walimu wa Sheria, nao watamhukumu auawe. |
19 |
Watamkabidhi kwa watu wa mataifa mengine ili adhihakiwe, apigwe viboko na kusulubiwa; lakini siku ya tatu atafufuliwa." |
20 |
Hapo mama yao wana wa Zebedayo alimjia Yesu pamoja na wanawe, akapiga magoti mbele yake na kumwomba kitu. |
21 |
Yesu akamwuliza, "Unataka nini?" Huyo mama akamwambia, "Ahidi kwamba katika Ufalme wako, hawa wanangu wawili watakaa mmoja upande wako wa kulia na mwingine upande wako wa kushoto." |
22 |
Yesu akajibu, "Hamjui mnaomba nini. Je, mnaweza kunywa kikombe nitakachokunywa mimi?" Wakamjibu, "Tunaweza." |
23 |
Yesu akawaambia, "Kweli mtakunywa kikombe changu, lakini kuketi kulia au kushoto kwangu si kazi yangu kupanga; jambo hilo watapewa wale waliowekewa tayari na Baba yangu." |
24 |
Wale wanafunzi wengine kumi waliposikia hayo, wakawakasirikia hao ndugu wawili. |
25 |
Hivyo Yesu akawaita, akawaambia, "Mnajua kwamba watawala wa mataifa hutawala watu wao kwa mabavu na wakuu hao huwamiliki watu wao. |
26 |
Lakini kwenu isiwe hivyo, ila yeyote anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote; |
27 |
na anayetaka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu. |
28 |
Jinsi hiyohiyo, Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu wengi." |
29 |
Yesu alipokuwa anaondoka mjini Yeriko, umati wa watu ulimfuata. |
30 |
Basi, kulikuwa na vipofu wawili wameketi kando ya njia, na waliposikia kwamba Yesu alikuwa anapitia hapo, walipaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!" |
31 |
Ule umati wa watu ukawakemea na kuwaambia wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaaza sauti: "Mheshimiwa, Mwana wa Daudi, utuhurumie!" |
32 |
Yesu akasimama, akawaita na kuwauliza, "Mnataka niwafanyie nini?" |
33 |
Wakamjibu, "Mheshimiwa, tunaomba macho yetu yafumbuliwe." |
34 |
Basi, Yesu akawaonea huruma, akawagusa macho yao, na papo hapo wakaweza kuona, wakamfuata. |